Sunday , 3rd Nov , 2024

Rais wa Kenya William Ruto, amekiri kuwepo kwa changamoto kubwa ya mauaji nchini kwake kufuatia mfululizo wa visa vya mauaji hasa ya wanawake na wasichana nchini humo, huku akisema kwamba kama Taifa inabidi suala la uhalifu na maadili liangaliwe kwa upana zaidi.

Rais wa Kenya William Ruto

Rais Ruto ametoa kauli hiyo leo Novemba 3, 2024, akiwa kanisani jijini Nairobi na kuonesha kusikitishwa juu ya kuendelea kwa uwepo wa mauaji hayo kila uchwao huku akisema kwamba Jeshi la Polisi nchini humo litawezeshwa ili kuweza kushughulikia changamoto hiyo.

"Ni kweli tuko na shida kubwa, vijana wetu haa wasichana wanauawa kiholela, watu ambao tungekuwa tunawaonesha mapenzi na kuwapenda sasa imekuwa ni mambo ya mauaji, inawezekana vipi wasichana na wanawake wa Kenya ambao wanatutarajia sisi tuwapende na sasa wanafia kwenye mikono ya wanaume. Kama Taifa tuna tatizo la uhalifu na maadili inabidi changamoto zote hizo mbili tuzitambue na kama serikali tutaviwezesha vyombo vya ulinzi na usalama vitendea kazi ili kuweza kukabiliana na mauaji haya," amesema Rais Ruto