Thursday , 31st Oct , 2024

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kwamba dira yake ni kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula barani Afrika kupitia mikakati mitatu mikuu ya serikali katika sekta ya kilimo. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akishiriki kwenye mjadala (round tables discussion) kuhusu Kilimo barani Afrika,

Hayo ameyabainisha akiwa nchini Marekani aliposhiriki kwenye mjadala kuhusu kilimo barani Afrika katika mji wa Des Moines, Iowa, Rais Samia amesisitiza kuwa serikali yake imejidhatiti kukuza sekta ya kilimo ili kufikia lengo hilo.

Miongoni mwa mikakati aliyoitaja ni uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji ambapo serikali imepanga kuwekeza katika miradi mikubwa ya umwagiliaji ili kuhakikisha ardhi nyingi zaidi inakuwa na uwezo wa kuzalisha mazao kwa mwaka mzima, kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza utegemezi wa mvua.

Katika hatua nyingine Rais Samia amesema mikakati mingine ni kuboresha upatikanaji wa teknolojia na pembejeo za kisasa ili kuongeza tija na ubora wa maza serikali inashirikiana na wadau wa maendeleo kutoa teknolojia za kisasa na pembejeo kwa wakulima jambo ambalo litawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kupata mazao bora yenye thamani kubwa kwenye masoko ya ndani na nje.

Aidha serikali imejipanga kukuza masoko ya mazao ya kilimo kwa kuweka mikakati ya kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini yanapata masoko ya ndani na nje, na hivyo kuwapa wakulima faida zaidi kutokana na juhudi zao.