Monday , 28th Oct , 2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George  Simbachawene ameonesha kukerwa na  baadhi ya Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi za Serikali  wenye  tabia ya kuwafokea Watumishi  walio chini yao  wakiamini kufanya hivyo ndio uongozi.

Amesema baadhi yao hudiriki hata kuwatukana watumishi huku akisisitiza kuwa jambo hilo ni kosa kubwa na kama kuna Kiongozi ana ufanisi lakini anafikia hatua ya kutukana watumishi, huyo hafai kabisa kwani zipo kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa umma za kuchukua kama mambo hayaendi sawa

Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) katika Kampasi ya Dar es Salaam ambapo amesema Kiongozi makini hahitaji kukasirika wala kufokafoka hovyo, cha msingi ni kuchukua hatua.

"Kuna watu walikuwa wanasoma kwa bidii zote ili wakipata nafasi kwenye utumishi wa umma wawakomeshe wenzao, kuna watu kazi yao kubwa ni kuwashughulikia watu na hiyo ndo raha yao" ameng'aka Simbachawene
Amesema mshahara hata uwe mkubwa kiasi gani kwa watumishi kama mahali pa kazi hakuna amani, kuna manyanyaso, hakuna kuthaminiwa na kutambuliwa kwa mchango wao hapawezi kuwa na ufanisi wa kazi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene ameitaka TPSC kutosubiri kuitwa kutoa mafunzo ya kujengeana uwezo mahali pa kazi bali watafute fursa pamoja na kuhakikisha  wanatoa mafunzo ya awali kwa watumishi wanapoanza kazi  ili waweze kutambua haki na wajibu wao.

Amesema kwenye Taasisi za Serikali kuna shida kubwa ya migogoro ya watumishi isiyoisha ilhali Chuo cha Utumishi kipo " nilitegemea kuona mnafika kwenye Taasisi hizo  kwa lengo la kutoa mafunzo kwa watumishi ili mambo yaende vizuri"

" Nimekuwa nikikutana na mashirika makubwa ya nje yakiniomba kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi katika Taasisi fulani za Serikali kwani wanaona mambo hayaendi sawa,  ninyi mpo lakini hamfanyi,  hii sio sawa,  changamkeni mna fursa nyingi za kubadilisha utumishi wa  umma nchini.

Amesema Chuo hicho kikiwa na utaratibu wa kutoa mafunzo kitasaidia watumishi wengi kutopelekana mahakamani au TAKUKUKURU kwa kuwa kutakuwa na maadili katika utendaji kazi.

Awali Mkuu wa Chuo Cha Utumishi wa Umma Tanzania na Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mchango mkubwa wa kutatua tatizo la watumishi katika Chuo ambacho kilikuwa kinakabiliwa na uhaba wa watumishi na hivyo kukwamisha kufikia malengo waliyojiwekea.