Saturday , 12th Oct , 2024

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amewataka Wamiliki na Wadau wa Vituo vya kufundishia Kiswahili Nchini kuchangamkia fursa ya kukopa fedha kwa riba nafuu kutoka Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kama ambavyo Wasanii wa Bongofleva na Waigizaji wanavyokopa

Akiongea na Wadau na Wamiliki hao Jijini Dar es salaam, Msigwa amewataka wajitahidi kufundisha kiswahili fasaha ili kupunguza  madhara ya kiswahili kuharibiwa Mitaani. 

“Vituo vyetu vya kufundishia kiswahili vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi hasa kupitia Wageni wanaojifunza lugha hii wakiwa na lengo kuelewa utamaduni wetu, kufanya biashara, uwekezaji, utafiti na kuunganisha juhudi za maendeleo Nchini, tunawapongeza Walimu kwa moyo wa kujitolea na kazi nzuri mnayofanya na inasaidia kueneza lugha Duniani”

“Serikali imejipanga kuwawezesha kuvianzisha vituo vya kufundishia kiswahili hata kwa mkopo wa riba nafuu, mikopo ipo kwa wenye sifa”

Mfuko wa Utamaduni na  Sanaa Tanzania umelenga kutoa mikopo yenye masharti nafuu ambapo hutolewa kwa Msanii mmojammoja, Vikundi au Makampuni yanayotengeneza kazi za sanaa, ambapo mikopo hiyo huanzia laki 2 hadi milioni 100 na  riba ya mkopo huo ni asilimia 9 tu inayotozwa katika salio la mkopo.