Thursday , 19th Sep , 2024

Waamuzi na Majaji 26 kutoka Tanzania wamefaulu mafunzo ya Kimataifa ya Waamuzi na Majaji wa Dunia wa IBA Nyota moja, mafunzo yalifanyika katika Chuo cha taaluma ya Polisi Dar es salaam kuanzia tarehe 6-11 August, 2024.

Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na Chama cha Ngumi cha Dunia (IBA) yalisimamia na wakufunzi Bi. Sadie Duffy kutoka Jamhuri ya Ireland ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Waamuzi na Majaji wa IBA na Ndugu Godavarisingh Rajcoomar kutoka Mauritius ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Waamuzi na Majaji wa Shirikisho la Ngumi Afrika (AFBC) na yalishirikisha jumla ya Waamuzi na Majaji 39 kutoka Tanzania (29), Kenya (8), Uganda (1) na Namibia (1).

Ni historia kubwa katika utawala wa Shirikisho chini ya Uongozi wa Rais Lukelo Willilo kuweza kuwaendeleza Waamuzi na Majaji kwa idadi kubwa kupata mafunzo na vyeti vya Kimataifa. 

Rais Willilo alinukuliwa amesema  "Tumewafungulia Dunia Waamuzi na Majaji wetu, kauli yangu ya siku zote ni ile ile, tunaendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi ya kuendeleza maendeleo ya mchezo wa Ngumi nchini, one step at a time. Ndoto yangu ni kuona Waamuzi wetu wakisimamia mashindano makubwa Afrika na Duniani."

Sasa Tanzania ina jumla waamuzi na majaji 27 wa Kimataifa wenye hadhi ya Nyota 1 ya Dunia wakitokea Uraiani, TPBRC, Polisi, Magereza, JKT na JWTZ.