Wednesday , 4th Sep , 2024

Tanzania imetajwa kuwa nchi kinara kwa Bara la Afrika ambayo kampuni za madini za Australia zimewekeza kwa asilimia 21% ya uwekezaji wote wa kwenye sekta ya madini.

Hayo yameelezwa leo Perth nchini Australia wakati wa mkutano wa Africa DownUnder (ADU) unaowashirikisha wadau wa madini kutoka Australia na nchi za Bara la Afrika.

Akihutubia mkutano huo kwa niaba ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan,Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amesema mikataba ya madini iliyoingiwa kwa miaka miwili iliyopita baina ya kampuni za madini za Australia na serikali ya Tanzania ina thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni 10 na hivyo utekelezaji wake utasaidia kuongeza mapato ya nchi, kuongeza nafasi za ajira,ushiriki wa Watanzania(Local Content) na kuchochea ukuaji wa sekta ya madini.

Aidha,Waziri Mavunde amezitaka kampuni hizo kuheshimu mikataba waliyoingina na serikali na hasa katika kunufaisha Watanzania kupitia wajibu kwa jamii(CSR),utoaji huduma na usambazaji wa bidhaa migodini na ulipaji wa kodi na tozo stahiki ili rasilimali hizo zitoe mchango katika maendeleo ya uchumi wa nchi na watu wake.

Wakitoa mawasilisho yao Watendaji wa Kampuni za Chief , Walkabout Resources,Peak Rare Earths ,Black Rock Mining  na Eco Graf kwa pamoja wameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na hivyo kuvutia uwekezaji huu mkubwa nchini ambao utachochea kukuaji wa kasi wa uchumi wa Tanzania.