Hukumu hiyo iliyosomwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita Kelvin Mhina, imesomwa kwa zaidi ya saa mbili ambapo Jaji Mhina ameeleza kuwa kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka mahakama imewatia hatiani washtakiwa wa kwanza hadi wa tatu na kumuachia huru mshtakiwa wa nne Musa Lubingo.
Waliotiwa hatiani katika kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023 ni Dayfath Maunga (30),Safari Labingo (54) na Genja Deus Pastory.
Jaji Mhina ameeleza kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo hakuna ubishani kuwa Milembe alifariki na mwili wake kukutwa na majereha kama ilivyothibitishwa na shahidi wa sita aliyekuwa daktari aliyeufanyia mwili uchunguzi.
Kuhusu mshtakiwa wa kwanza shahidi namba 11 ambaye ndiye aliyeandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa alikiri kupanga ,kutafuta wauaji na alikiri kuishi na marehemu kama mume na mke na kuwa alikuwa ananyanyaswa na alitaka kuondoka lakini ilishindikana.
Akitoa hukumu hiyo jaji Mhina ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria washtakiwa hao wanahukumiwa kunyongwa hadi kufa na kuwaeleza kuwa wana haki ya kukata rufaa endapo hawajaridhika na hukumu hiyo.