Akizungumza Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Agosti 5, 2024 ambapo watu hao ambao idadi yao ilikuwa ni 23 walikuwa wakitoka kusherehekea kilele cha wiki ya mwananchi iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyoisha.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, katika ajali hiyo ambayo chanzo chake hakijajulikana ilisababisha mtu mmoja kufariki dunia, watano hawajulikani huku wengine 17 wakinusurika baada ya wavuvi waliokuwa karibu na eneo hilo kuwaokoa.
"Watu hao walikuwa wanasafiri kutoka kisiwa cha Yozu kuelekea Kijiji cha Itabagumba kilichopo kata ya Bulyaheke wilayani Sengerema ndipo mtumbwi huo ulipoanza kuingia maji na kuanza kuzama," amesema Mutafungwa
Hatahivyo Kamanda Mutafungwa amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi, wavuvi na timu ya uokoaji inaendelea na zoezi la kuisaka miili hiyo.