Wednesday , 31st Jul , 2024

Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali inatambua na kuthaminiu mchango wa watumishi katika sekta ya afya huku akisema itaendelea kuboresha maslahi yao polepole

Rais Samia amesema hayo katika kongamano la kumkumbuka Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamin Mkapa ambapo lilijikita zaidi kuangalia maendeleo katika sekta ya afya

"Suala la maslahi kwa watumishi kwenye sekta ya afya tutaendelea nalo polepole, tutapunguza leo hiki, kesho hiki keshokutwa hiki, sitaki kuahidi kwamba tutaangalia kwa mwaka mmoja lakini niseme tunathamini kazi yenu tunajua ugumu wa kazi yenu na tutaangalia maslahi yenu"

Kuhusu uongozi wa Hayati Mkapa Rais Samia amemtaja kama kiongozi aliyekuwa na maono makubwa na aliyeongoza mageuzi mbalimbali serikalini 

"Hayati Mzee Mkapa alikuwa kiongozi wa maono makubwa, na aliyekuwa na ujasiri wa kukabiliana na mambo magumu, katika sekta ya afya suala la nguvu kazi ya afya ni jambo moja gumu sana, ni suala gumu kwa sababu halina matokeo ya haraka, ni rahisi zaidi kuwekeza katika miundombinu ya afya, vifaa tiba na madawa kuliko kuwekeza kutengeneza nguvu kazi" 

"Kujenga kituo cha afya kunaweza kukamilika ndani ya mwaka mmoja ikiwa fedha zipo, wakati unahitaji miaka sita kumuandaa daktari mmoja, na walau miaka mitatu kumuandaa muuguzi mmoja, hapo hatujazungumzia madaktari bingwa ambao huchukua takribani jumla ya miaka tisa hadi 12 kumuandaa mmoja" 

"Mzee Mkapa aliingia madarakani katika kipindi ambacho UKIMWI ulikuwa umeshika kasi sana hapa nchini, taifa lilipoteza nguvu kazi kubwa, familia zikatetereka, kukawa na ongezeko kubwa la watoto yatima, nikivuta taswira ya hali ilivyokuwa napata majibu kwanini Mzee Mkapa anakumbukwa na anapaswa kuendelea kukumbukwa kwenye sekta ya afya" 

Katika kipindi cha uongozi wake Mzee Mkapa alianzisha tume ya kudhibiti UKIMWI yani TACAIDS, mfuko wa bima ya afya, mageuzi ya kimuundo katika hospitali ya taifa ya Muhimbili yaliyozaa taasisi ya mifupa MOI, na uboreshwaji wa mazingira ya kazi maeneo ya pembezoni mwa nchi ili kuvutia wataalam wa sekta ya afya kufanya kazi na kubaki maeneo ya pembezoni" amesema Rais Samia