Thursday , 22nd Feb , 2024

Makamo wa Rais Dkt. Philip Mpango amemwagiza Naibu Waziri wa Viwanda Exaud Kigahe kuhakikisha wanakuwa na mpango mfupi wa kusaidia wakulima wa matunda wa mkoa wa Tanga matunda yao yasiharibike shambani.

Makamo wa Rais Dkt. Philip Mpango

Dkt Mpango ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Kabuku aliposimama kwa muda wakati wa ziara yake ya siku tatu Mkoani Tanga. 

"Mkuu wa mkoa (Waziri Kindamba) na timu yako mkishirikiana na Wizara ya Viwanda fanyeni tathimini ya mazao mnayozalisha, lakini nikuagize Naibu Waziri kuweni na mpango wa muda mfupi kuwasaidia wananchi hapa muombeni mkurugenzi wa kiwanda cha Jambo aje Tanga anunue matunda ya wananchi hawa," alisema Makamo wa Rais Dkt. Mpango 

Kuhusu ubovu wa barabara aliolamikiwa na diwani wa kata ya Kabuku Abdallah Pendeza, Naibu Waziri wa Tamisemi Deogratius Ndejembi, alisema serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan iliongeza bajeti ya barabara kwa TARURA kutoka shilingi bilioni 226 hadi kufikia bilioni 810  kwa ajili ya kuzisaidia barabara za vijijini na mkoa wa Tanga umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 40 kutoka bilioni 12 za awali.

"Mheshimiwa Makamo wa Rais meneja wa TARURA wa wilaya ya Handeni tumemwingizia kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya kukabiliana na barabara za vijijini ambazo zimeharibika na mvua" alisema Ndejembi 

Naye Naibu Waziri wa ujenzi Godfrey Kasekenya aliagizwa na Makamo wa Rais kufuatilia mkataba wa mkandarasi wa kampuni ya Kichina ya Hennan Highway ambayo tangu ipewe kazi ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Handeni, Kibirashi, Kiteto, Kondoa hadi Singida wanasuasua.

Mbunge wa Handeni mjini Reuben Kwagwila alimuomba Makamo wa Rais kusaidia kumsukuma mkandarasi huyo ambaye miezi 26 sasa tangu alipopewa kazi ya kujenga barabara hiyo hajaweka hata kilimeta moja ya lami.

Naibu wa Waziri wa ujenzi, alisema Waziri wa ujenzi Dkt Inocent Bashungwa aliitembelea barabara hiyo na kumpa muda hadi mwezi machi mwaka huu wawe wametafuta fedha za kujenga barabara hiyo vinginevyo serikali itavunja mkataba wao.

Makamo wa Rais atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mauzo ya hatifungani Kwa ajili ya kugharamia miradi ya maji Jiji la Tanga kisha mchana ataelekea wilayani Mkinga kuzindua Chuo cha Veta katika wilaya hiyo.