Thursday , 8th Feb , 2024

Wakulima wa zao la mkonge mkoani Tanga, wameiomba serikali kuingilia kati hatua ya mnunuzi mpya 'WEFARM' kushindwa kununua mkonge na kusababaisha maisha yao kuwa magumu.

Malalamiko hayo yanatoka kwa wakulima wa mashamba matano ya Magoma, Mgombezi, Hale, Mwelya na Magunga.

Wakulima hao pia wameilalamikia Bodi ya Mkonge kwa kushindwa kumchukulia hatua mnunuzi huyo ambaye ameshindwa kutekeleza matakwa ya mkataba kwa kununua mkonge wote.

Mwakilishi WEFARM aliyetambulishwa kwa jina moja la Revocatus alipoulizwa kuhusu kampuni yake kushindwa kununua mkonge kwa mujibu wa mkataba, alijibu “hayo mambo waulize Bodi ya Mkonge.” 

Alipoulizwa Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge Saddy H. Kambona kuhusu malalamiko hayo alisema, “sijajua kwa sababu mimi nilikuwa nilikizo.” 

Kambona alipoulizwa sababu za ofisi yake kushindwa kumchukulia hatua mnunuzi huyo, alisema “taarifa kwetu hazijafika, vyama havileti taarifa.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Mgombezi (Mgombezi Amcos), Rashid Msemo amekiri kuwepo kwa tatizo la ununuzi wa mkonge.

“Ni kweli kuna kilio kikubwa cha wakulima, kukataa hili nitakuwa nimesema uongo. Tatizo hilo limesababisha kazi za vyama kusimama. Marobota yamejaa kwenye maghala,” alisema.

Mwenyekiti wa wenyeviti wa vyama vya ushirika vya mkonge Tanga, Shadrack Lugendo alisema malalamiko hayo yapo na mnunuzi bado hajaweza kununua mkonge wote uliopo ghalani.