Wednesday , 7th Feb , 2024

Zaidi ya shilingi bilioni 37 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya kwenye vituo vya afya na zahanati zilizopo vijiji lengo ikiwa ni kuisaidia jamii katika mapambano ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi runinga 57 zitakazotumika katika kutoa elimu ya kupambana na maradhi kwenye vituo hivyo na zahanati ili zisaidie kuielimisha jamii dhidi ya mapambano ya magonjwa hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Thomas Rutachunzibwa  amesema uwepo wa umeme kwenye maeneo hayo umesaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya.

Kwa upande wake, Afisa uhusiano wakala wa nishati vijijini (REA) Jaina Msuya amesema waliona upo umhimu wa kusambaza umeme vijijini ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Amesema kupitia mradi huo wa kusambaza umeme katika vituo vya afya na pampu za maji vijijini umefanikiwa kuvifikia vituo vya afya 57 pamoja na pampu za maji 353 ambazo zinagharimu Zaidi bilioni 37.4
Mwakilishi kutoka wizara ya afya, James Mhilu amesema umhimu wa kupeleka huduma ya umeme na maji vijijini unasaidia katika mapambano ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu, uviko-19 na magonjwa mengine ya mlipuko.

Pia amesema mradi huo utasaidia utoaji wa huduma za afya kwa wananchi ikiwemo kupata chanjo na vipimo vingine vya maabara na utunzaji wa takwimu.

“Vile vituo vya afya ambavyo vilikuwa vinafunga saa 12 sasa vitalazimika kufanya kazi kwa masaa 24 lakini uwepo wa umeme utaongeza idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa lakini suala la utunzaji wa kumbukumbu,”amesema Mhilu