Tuesday , 6th Feb , 2024

Katika hali isiyokuwa ya kawaida mbuzi 17 wamekutwa katika pori lililopo mtaa wa Bombambili Halmashauri ya mji wa Geita wakiwa wamekufa huku chanzo cha mbuzi hao kufa kikiwa hakijafahamika.

Wakizungumza na EATV mashuhuda waliofika katika eneo hilo wamesema licha ya taarifa hizo kusambaa kwa watu wengi mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyejitokeza kuwa ndiye mmiliki wa mbuzi hao.

“Nilipofika pale nikafikiri mbuzi hao ni wakwangu lakini nilivyochunguza hawakuwa wakwangu baada ya hapo nikampigia mwenyekiti wa mtaa ili aje kuona tukio hilo kwaiyo alifika pamoja na polisi jamii wakawa wanauliza mbuzi hawa ni wanani lakini mpaka sasa hatujui mbuzi hawa ni wanani” Maneno Lusota Kanyeti amesema Mkazi wa Bombambili

“Nilifika hapa asubuhi maana nilipewa taarifa kuwa kuna mbuzi zimekufa basi nilifika nikaona ila hatujajua nini kimesababisha mbuzi hawa wafe maana hazina hata damu kusema zimechinjwa wala nini labda tumekuta zimekufa arafu zimeachanishwa achanishwa” Teddy Mihayo - Mkazi wa Bombambili

“Inaonekana mbuzi hizi zimebebwa zikawekwa maana kama pengine tuseme zimekula mazao ya watu zisinge kuwa huku porini zimekufa zikiwa sehemu moja hivi arafu mafungumafungu” - Meshaki Julius, Mkazi wa Bombambili
Aidha wakazi wa mtaa huo wameliomba jeshi la polisi kwa kushirikiana na wataalamu wa mifugo kufanya uchunguzi ili kujua sababu ya mbuzi hao kufa ili kuondoa wasiwasi kwa wakazi wa mtaa huo.

“Tunaomba polisi kitengo cha mifugo kufanya uchunguzi wa kina ili kujua nini kimesababisha mbuzi hawa kufa ili kwa wananchi watuondolee wasiwasi na taharuki iliyopo kwenye jamii na mpaka sasa kuna baadhi ya mbuzi wamesha hamishwa hawapo sasa hatujui wamepelekwa wapi” Doto Kasala Gidion - Mkazi wa Bombambili

“Sisi kama wafugaji tunafuga tukiwa na malengo ya kufanya kitu flani sasa ikitokea majanga kama haya jamani kwakweli inauma sana” Maneno Lusota Kanyeti - Mkazi wa Bombambili

Afisa Mtendaji wa Kata ya Bombambili Cosmas Bayaga amefika eneo la tukio huku akisema jitihada za kumtafuta mmiliki wa mbuzi hao bado zinaendelea.

 “Tulifika hapa pamoja na polisi jamii na baadae wakaja polisi kata wa kata ya kalangalala wakawajulisha na polisi kitengo cha mifugo na mpaka sasa hatujampata mmiliki wa mbuzi hao kwaiyo tunaendelea kuwasiliana na jamii jirani ili tufahamu mbuzi ni wanani ili aweze kuisaidizana polisi ili kujua chanzo vifo vyambuzi hawa ni nini” Cosmas Bayaga - Afisa Mtendaji wa Kata ya Bombambili

Jeshi la polisi kwa kushirikiana na Kitengo cha mifugo halmashauri ya mji wa Geita waliondoka na sampuli kwaajili ya uchunguzi na tayari wameanza zoezi la kuzika mizoga ya mbuzi hao.