Tuesday , 6th Feb , 2024

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema wizara yake itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inakua kwa kuboresha mialo ya samaki wa maji baridi na maji chumvi ili kupata samaki bora zaid

Prof. Shemdoe amebainisha hayo leo (05.02.2024) jijini Dodoma kando ya kikao cha katibu mkuu huyo na wakurugenzi wa halmashauri majiji, manispaa na wilaya zenye shughuli za uvuvi ili kuweka mikakati zaidi ya namna ya kufanya shughuli hiyo kuwa endelevu.

Amesema kutokana na maagizo aliyotoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni jijini Mwanza wakati wa kukabidhi boti za uvuvi na vizimba ya kuitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na TAMISEMI katika kukuza Sekta ya Uvuvi, tayari maelekezo hayo yameanza kufanyiwa kazi ili kufikia maono ya Mhe. Rais.

“Leo hii tumekaa kutekeleza kimsingi maelekezo ambayo Mhe. Rais ameyatoa na tumepata wasaa kuongea na wakurugenzi wa halmashauri na kupanga mipango namna bora ya kuimarisha maeneo ya kupokelea samaki.” Amesema Prof. Shemdoe

Ameongeza kuwa baada ya kikao hicho kutakuwa na matokeo chanya yakiwemo ya kupatikana kwa bidhaa bora za samaki ambao watakuwa wanahitajika zaidi kwenye viwanda vya kuchakata minofu ya samaki hivyo kufanikisha zaidi masoko ya ndani na nje ya nchi.

Awali akifungua kikao hicho Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Nazael Madalla amesema Sekta ya Uvuvi imekuwa moja ya chanzo muhimu cha mapato kwa halmashauri na taifa kwa ujumla pamoja na kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na kuwa kichocheo kikubwa cha uwekezaji.

Ameongeza kuwa kufuatia sekta hiyo kuwa muhimu viwanda vya kuchakata minofu ya samaki vimekuwa vikihitaji samaki kwa wingi kwa ajili ya kuchakata na kusafirisha minofu ya samaki katika masoko ya nje ya nchi ambayo yanaliingiza taifa fedha za kigeni, hivyo ni muhimu kuzilinda rasilimali za uvuvi na kuziongezea thamani.

Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho wamesema Sekta ya Uvuvi ni muhimu sana katika halmashauri wanazotoka kwa kuwa sekta hiyo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa ajira na watu wengi wamekuwa wakiishi kwa kutegemea uvuvi.

Wamesema kupitia kikao hicho watapata fursa ya kufahamu zaidi na namna bora ya kuboresha mialo ya kupokelea samaki, ikiwemo miundombinu ya kuhifadhia samaki ili kuyaongeza thamani mazao ya uvuvi.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kukutana na wadau mbalimbali kufuatia maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka Sekta ya Uvuvi kurasimishwa ili wananchi wanaofanya shughuli zao kupitia sekta hiyo waweze kutambulika rasmi na waweze kunufaika kupitia taasisi mbalimbali za kifedha.