Tuesday , 12th Dec , 2023

Katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bw. Lawrence Mafuru amewataka watanzania kushiriki katika mchakato wa kutoa maoni ili kuandaa dira ambayo italisaidia taifa kupiga hatua katika kuyafikia malengo ya kimaendeleo ambayo imepanga.

Akizungumza katika mjadala wa kitaifa wa miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 leo Disemba 12, 2023 kupitia mtanado (Zoom) Bwana Mafuru amesema kwa sasa wananchi wanapaswa kutambua kuwa dira inayoandaliwa siyo kwaajili ya viongozi wa Serikali bali ni kwaajili ya Watanzania wote.

"Tumekuwa mafundi wa kutoa maoni pembeneni, sasa tutumie fursa hii kutoa maoni ya Tanzania ipi tunayoitaka, Tume iko wazi muda wote na hata wale wanaotaka kuja kutoa maoni yao moja kwa moja wanakaribishwa mwisho wa yote tutatakiwa kushirikiana kwa pamoja" alisisitiza Bw. Mafuru. 

Awali akizungumzia kuhusu hali ya maisha ya Mtanzania kwa sasa na Bw. Mafuru amebainisha kuwa kiwango cha umaskini kimepungua hadi asilimia 9% kwa kipindi hiki ilikinganishwa na miaka ya 2000 ambapo umaskini uliokithiri ulikuwa kwa asilimia 19%

"Pengine tungekuwa tumeenda mbele zaidi, tumerudi nyuma kidogo kutokana na janga la COVID 19 ambalo hatukuwa tumejipanga kukabilian nalo kama yalivyokuwa majanga mengine" alisema Bw. Mafuru

Kuhusu kukua kwa uchumi wa Tanzania, Bw. Mafuru amesema uchumi umekuwa ukikua kwa kiasi kikubwa ambapo kwa kipindi cha miaka ishirini iliyopita uchumia umekua  kwa wastani wa asilimi 6% ukilinganisha na mataifa mengine hata mataifa makubwa yaliyoendelea na kwamba lengo la serikali lilikuwa ni kukuza uchumi kwa asilimia 8% hivi na zaidi

"Tumeweza pia kukua bila kutegemea sekta moja ya uchumi, nchi yetu ina sekta nyingi za uchumi ambazo ziko balanced kwahivyo hakuna namna ikitetereka sekta moja inaweza kuathiri uchumi kwa ujumla, tumejenga misingi imara kwenye uchumi mbalimbali ziko sekta zinazokua haraka na ambazo hazikui haraka na zinachangia"  Bw. Lawrence Mafuru

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imezingatia ushirikishwaji wa makundi yote ya jamii kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kushiriki kwa kutoa maoni yake katika kuandaa mipango ya nchi kwa miaka 25 ijayo.

“Tarehe 9 Desemba tumefanya Mkutano wa Dira ambao tulihakikisha makundi yote ya jamii yanaalikwa na kuhudhuria mkutano ule, vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa hapa nchini vilialikwa na kushiriki kama ambavyo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekua akisisitiza kila Mtanzania kushiriki”, amesema Prof. Mkumbo.