Saturday , 18th Nov , 2023

Katibu wa Bunge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi ofisi ya Bunge Nenelwa Mwihambi, ndc amehairisha kikao cha Baraza la Wafanyakazi ofisi ya Bunge baada ya kusoma na kuridhia maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho.

Kikao hicho kimehairishwa leo tarehe 18 Novemba, 2023 katika hoteli na kituo cha Mikutano cha APC kilichopo Mbweni Jijini Dar es Salaam.

Maazimio mbalimbali yalifikiwa katika kikao hicho ikiwemo kuendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango kazi wa ofisi ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 yanatimia na baada ya mpango wa maendeleo wa Taifa kupitishwa na Bunge idara na vitengo vianze mchakato wa kuweka vipaumbele katika kutenga Bajeti hususan kwa miradi ya inayoendelea. Aidha, kwa miradi mipya maandiko ya miradi ikamilike na yapitishwe katika hatua zote muhimu za maamuzi kabla ya kutenga Bajeti.

Akizungumza wakati wa kikao hicho mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Sekta ya Afya (TUGHE) Taifa ambaye ni Mjumbe wa Kamati kuu TUGHE Taifa, Ndg. Brendon Maro amempongeza Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson kwa ushindi alioupata wa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

“Ushindi wake umekuja kwa kuwa ana mtandao mmoja kutoka kwenye taasisi yake anayoifanyia kazi hasa watumishi wamesaidia sana”amesema Maro

Awali, akizungumza wakati akihairisha kikao hicho Katibu wa Bunge, Ndg. Nenelwa Mwihambi, ndc ameshukuru kwa salamu hizo zilizotolewa na TUGHE Taifa kwa Mhe. Spika na kuhaidi kumfikishia, Pia alihimiza watumishi wafanye kazi kwa bidii ili ilete tija kwa Bunge na Taifa.

Kikao hicho cha muda wa siku mbili kimeanza jana tarehe 17 Novemba, 2023 na kimehitimishwa leo tarehe 18 Novemba, 2023.