Wednesday , 15th Nov , 2023

Balozi Abdallah Kilima ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amekanusha uvumi ambao umekuwa ukienezwa kuwa Watanzania wengi wanaofanya kazi katika nchi za Mashariki ya Kati wanateswa.

Balozi Abdallah Kilima ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Akizungumzia manufaa yanayotokana na mkataba uliosainiwa kati ya Tanzania na Saudi Arabia ambao utawawezesha Watanzania kupata ajira katika sekta mbalimbali amesema, asilimia 92 ya wanaofanya kazi kwenye nchi hizo wananufaika, na asilimia nane iliyobaki wanaweza kuwa wanapitia changamoto mbalimbali kutokana na kutofuata taratibu.

"Kumekuwa na suala ambalo limejengeka mitandaoni kwamba watu wengi wanateseka na kunyanyasika wanapokuwa Uarabuni, na weza kusema kwamba kwa asilimia 92 habari hizi si za kweli, wapo watu wanafanya kazi katika mazingira mazuri na kipato chao wanachokipata ni kikubwa," amesema Balozi Kilima

Aidha ameongeza kuwa, "Oman kuna Watanzania 25000 wanafanya kazi, na kati yao takribani elfu 17 wanafanya kazi za ndani na utaona kabisa kwamba uwepo wao kwa wingi unathibitisha kwamba mazingira yao ya kufanya kazi ni salama na wanaendelea kufanya kazi, na ni lazima nikiri ndiyo maana nikasema 92% habari hizo si za kweli, katika 8% tunakubali kwamba ziko changamoto ambazo ni za kawaida na zinawakuta wale ambao wamepita nje ya mfumo uliowekwa," 

Balozi Kilima amesisitiza kuwa nchi nyingi za Mashariki ya Kati zinategemea nguvu kazi kutoka nje, hivyo ni wakati sasa kwa Tanzania kuchangamkia fursa hiyo, huku akiongeza kuwa zipo nchi nyingjme tatu ambazo zimeomba kusaini mkataba kama huo na Tanzania ili kupata nguvu kazi.

Ameongeza kuwa Saudia Arabia inatarajiwa kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2034, na inaweka mikakati ya kuandaa maonesho ya kibiashara (Expo) mwaka 2030, hivyo ni wakati mwafaka kusainiwa kwa mkataba huo ambao utatoa ajira kwa maelfu ya Watanzania.