
Akizungumza katika ziara ya siku moja hivi karibuni katika Hifadhi ya Taifa Arusha Afisa Ustawi wa Hospitali ya Kibong' oto Wazo-Eli Yohana Mshana amesema mradi wa kuwatoa wagonjwa wa kifua kikuu sugu (MDR) kutalii ni wa kwanza katika hospitali hiyo ambapo mpaka sasa wamewapeleka wagonjwa 76.
"Ukitia fursa hizi za kuwaleta wagonjwa katika vivutio vya mbuga hizi tumezianza na sasa takribani tunaenda kufikisha wagonjwa 76. Wale ambao wamepata bahati ya kutoka wameimarika sana kisaikolojia" amesema Mshana.
Kwa upande wake Mratibu wa Kifua Kikuu Sugu Hospitali ya Kibong' oto Dkt. Happiness Mvungi amesema wagonjwa wanakaa katika vitanda kwa muda mrefu hatua ambayo imekuwa ikiwachosha na kuwafanya wakate tamaa ya kupona.
"Matibabu ya Kifua Kikuu Sugu ni ya muda mrefu unakaa na wagonjwa kwa muda mrefu wakiwa wodini, kitendo cha wao kuja outing kinasaidia wao kurelax lakini pia kufuatilia matibabu yao kwa ufasaha zaidi" alisema Dkt. Mvungi.
Pia katika ziara hiyo wagonjwa wa kifua kikuu sugu walifanya mazoezi katika Hifadhi ya Taifa Arusha chini ya Muuguzi na Msaidizi wa Daktari wa Mazoezi Kalista Mrina.
"Najua mgonjwa anafaidika kwa kubadilisha hali ya hewa kwasababu wamekaa hospitali muda mrefu na alikotokea alikuwa hana hii fursa ya kutembelea mazingira kama haya" amesema Muuguzi Mrina.
Wagonjwa wa Kifua Kikuu Sugu wameipongeza serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan, hospitali ya Kibong' oto na wadau mbalimbali waliochangia wao kupata matibabu hayo.
"Nimefurahi kufika katika mbuga hii nimejifunza vitu vingi kiasi kwamba nikienda mtaani nitaenda kuwaelezea wenzangu mengi mazuri niliyoyapata katika mbuga hii, nimpongeze mama yetu (Rais Samia Suluhu Hassan) na mkurugenzi wetu (Dkt. Leonard Subi)" alisema Magdalena Japhet, mkazi wa Muheza, Tanga.
Mbali na hilo Mshauri Mkuu wa Taasisi Afya ya Mapafu na Moyo kutoka nchini Norway (LHL International), Laila Lochting amesema wameamua kupanua ushirikiano wao na Kibong'oto ikiwamo madawa hadi kuwafanyia matibabu ya kisaikolojia ambapo kwa kuanza wameanza na utalii wa ndani wa vivutio vilivyopo Tanzania.
"Tunachokifanya kwa sasa ni mojawapo ya sehemu katika mradi katika ushirika wetu na Kibong'oto tukijitahidi kuboresha maisha ya wagonjwa wetu ambao wanakaa hospitalini kwa miezi mingi." alisema Lochting.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikadiria kuwa watu 456,000 mnamo mwaka 2019 waliambukizwa Kifua Kuku Sugu (MDR-TB) na waliopata matibabu walifikia 177,000 ambapo ni asilimia 56 walipona maradhi hayo.