Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Asha–Rose Migiro
Akizungumza na viongozi wa Tume hiyo jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Asha–Rose Migiro alisema Serikali ina wajibu wa kuzingatia haki za binadamu katika utekelezaji wa majukumu yake na hivyo na hivyo ni muhimu kwa Tume kuibua na kutoa taarifa juu ya masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
“Serikali ina wajibu wa kufanya kazi kwa kuzingatia na kulinda haki za binadamu ili wananchi waweze kuwa na amani katika nchi yao,” alisema Dkt. Migiro katika mikutano wa viongozi wa Tume hiyo uliohudhuriwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Ummy Mwalimu. Waziri Migiro alikuwa katika ziara ya kubadilishana mawazo na uzoefu na viongozi wa Tume hiyo.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilianzishwa mwaka 2000 na kuanza kazi rasmi mwaka 2002 ili, pamoja na majukumu mengine, kutoa ushauri kwa serikali na vyombo vingine vya umma na vya sekta binafsi kuhusu haki za binadamu na utawala bora.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri alisema ni muhimu kwa Tume hiyo kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa umma kuhusu uzingatiaji wa haki za binadamu na utawala bora kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuwafikia wananchi wengi kwa kasi na haraka.
“Katika nchi yetu suala la teknolojia ya mawasiliano na habari ni muhimu sana ili kufikisha ujumbe kwa wananchi kwa kasi na kwa haraka zaidi, ongezeni kasi ya kuitumia,” Naibu Waziri aliwaambia viongozi hao walioongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Wakili Bahame Tom Nyanduga.
Kwa upande, Mwenyekiti wa Tume hiyo aliwashukuru Waziri na Naibu Waziri kwa ziara yao kwa Tume na kuahidi kutekeleza maelekezo waliyopewa pamoja na changamoto zilizopo.
Aidha, Wakili Nyanduga alisema kuwa Tume yake ina mpango wa kuandaa programu ya kuelimisha umma juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuwa wao pia wana haki ya kuishi.
“Kuwaua watu wenye ulemavu wa ngozi ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwa vile wao pia wana haki ya kuishi,” alisisitiza Mwenyekiti huyo na kufafanua kuwa Tume inaandaa mpango wa kuelimisha umma ili kukomesha mauaji hayo.
Pamoja na Mwenyekiti wa Tume, mkutano huo ulihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti Bw. Iddi Ramadhani Mapuri, Makamishna Tume hiyo Bw. Mohammed Khamis Hamad, Dkt. Kevin Mandopi, Bi. Rehema Msabila Ntimizi, Bi. Salma Ali Hassan, Katibu Mtendaji wa Tume Bi. Mary Massay na viongozi wengine wa tume.