Wednesday , 19th Jul , 2023

Mtoto Sixtus Kimario (7) mkazi wa Kijiji cha Samanga, wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro na mwanafunzi wa darasa la kwanza, amefariki dunia Julai 17, 2023, kwa kupigwa na mwalimu wake kwa kile kinachodaiwa kupiga kelele na kujisaidia haja ndogo darasani.

Samanga

Wanakijiji ambao wamekusanyika nyumbani kwa wazazi wa marehemu Sixtus Kimario aliyekuwa akisoma Shule ya Msingi Samanga wamemtaja Mwalimu James Urassa kutenda ukatili huo na kwamba amekimbia kusikojulikana.

EATV imezungumza na Mama wa Marehemu Venosa Kimario na kusema taarifa za kufariki kwake alizipata kutoka kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Samanga wakidai Mwalimu Urassa alianza kuwapiga darasa zima kutokana na kupiga kelele.

"Sasa huyo wa kwangu alipoanza kumchampaakawa amejikojolea, akamnyanyua kwa mara ya pili, akamwambia unajikojolea unachafua darasa akampiga kwenye usogo hapa na mgongoni, mtoto akawa ameanguka, akabakia hapohapo," amesema Mama wa marehemu.

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ambapo mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa siku chache zijazo baada ya uchunguzi kukamilika.