Saturday , 21st Feb , 2015

Vijana nchini Tanzania wamehamasishwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kuweza kushiriki kikamilifu katika upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu hapa nchini.

Mkuu wa Idara ya Uenezi Taifa wa chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini CHADEMA Bw. Waitara Mwita ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salaam wakati wa mafunzo kwa viongozi waCHADEMA waliochaguliwa kuwa wenyeviti wa serikali za mitaa.

Bw. Waitara amesema wakati umefika sasa kwa vijana kushiriki kikamilifu katika masuala ya uchaguzi ili kuleta maendeleo hapa nchini na kuondokana na dhana kwamba suala la kushiriki katika kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ni kwa ajili ya wazee pekee.

Amesema iwapo vijana watashiriki ipasavyo taifa litakuwa na mwamko kwa kuwa vijana hao wataweza kuwaelimisha wengine namna gani wataweza kujitokeza na kujiandikisha kwa lengo la kutimiza haki yake ya msingi.