
Wakizungumza na #EATV wakazi wa kata Kashai wamesema kuwa vijiwe vya kuuza mishikaki katika kata hiyo vimeongezeka na kuomba serikali kuwakagua watu wote wanaouza mishikaki ili kujiridhisha kama wana uthibitisho na vibali na pia kujihakikishia kama nyama inayouzwa huko ina mihuri ya mamlaka husika.
“Inawezekana na mimi nimeishakula nyama ya mbwa mitaani, mamlaka husika zinapaswa watu wanapofungua vijiwe vya mishikaki wakaguliwe, hiki sio kitendo kizuri na hatujui kama kweli ilikuwa kwa matumizi yake, inawezekana ana connection na mtu nyama zinapelekwa usiku na tunauziwa” amesema Kamugisha.
Diwani wa kata Kashai Ramadhan Kambuga amesema tukio hilo ni la pili katika kata yake, na kuwataka wananchi kuacha tabia ya kununua nyama mitaani, na badala yake wanunue nyama katika maeneo rasmi, huku akimkana mtu huyo ambaye jina lake halikufahamika haraka, kuwa hamfahamu kama ni mkazi wa kata hiyo
Kwa upande wake mchungaji Elisha Bililiza wa kanisa la Anglikana Bukoba, akizungumzia tukio hilo amesema kufanya hivyo ni ukosefu wa uadilifu, na kuiasa serikali kuwafuatilia watu wanaofanya vitendo vya namna hiyo, maana wanaweza kusababisha athari ya magonjwa kwa wananchi.
Afisa mifugo wa manispaa ya Bukoba, Viviano Musigula amesema uchinjaji wa nyama unafanyika katika machinjio rasmi, na kwamba mifugo hukaguliwa kabla ya kuchinjwa, lakini akadai kuwa mbwa sio mnyama rasmi kwa kuliwa na binadamu.
“Katika jamii yetu ya Kitanzania hata jamii unayoishi wewe nafikiri mbwa sio mfugo kwa ajili ya kitoweo, ni kwa ajili ya ulinzi na wengine wanafuga kama mapambo nyumbani, kwa hiyo sio kitoweo na kwenye orodha ya wanyama wanaoliwa mbwa hayumo.” Amesema Musigula.
Hata hivyo katika hali isiyo ya kawaida, kabla ya baba huyo aliyedai nyama hiyo ni kwa ajili ya kitoweo chake nyumbani kuchukuliwa na polisi, alitafuna nyama mbichi ya mbwa mbele ya wananchi.