Uongozi wa mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na bodi ya shule ya sekondari ya Idodi mkoani humo wamewarudisha nyumbani watoto 190 wa kidato cha pili na cha nne ambao bweni lao lilishika moto na kuungua hapo jana na kuteketeza vifaa vyao vyote.
Maamuzi hayo yamefanyika ili kupisha maandalizi ya kutafuta mahali pa kuwahifadhi kwa muda wakati ufumbuzi wa kudumu wa tatizo lao ukiendelea kutafutwa.
Moto huo uliozuka majira ya saa nne na nusu asubuhi wakati wanafunzi wakiwa darasani uliteketeza bweni hilo linalokaliwa na wasichana wa kidato cha pili na cha nne shuleni hapo na kuwaacha wanafunzi hao wanaojiandaa na mitihani ya kidato cha pili na ule wa kumaliza kidato cha nne wakiwa hawana pa kulala lakini zaidi hata vifaa yakiwemo madaftari yaliyojaa notes zao nayo yameteketea
Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza ameuagiza uongozi na bodi ya shule hiyo kumleta mtaalam wa mfumo wa umeme ili aweze kukagua mfumo wa umeme wa shule hiyo.
Naye mwenyekiti wa bodi ameeleza kuwa kutokana na tukio hilo wameamua pamoja na mambo mengine kuwaondoa shuleni hapo wanafunzi 192 waliounguliwa na vifaa vyao pamoja na kuwahamisha kwa muda wale wengine ambao bweni lao lilinusurika na moto huo lakini vifaa vyao vingi vikiharibika wakati wa zoezi la uokoaji
Hii ni mara ya pili kwa bweni la wasichana kuteketea kwa moto katika shule ya sekondari idodi ndani ya kipindi cha miaka mitano ambapo mwaka 2009 bweni lingine la wasichana katika shule hiyo hiyo liliungua moto usiku wa manane na kuteketeza wasichana 12 waliokuwa wamelala kwenye bweni hilo kiasi cha kutotambulika.