Thursday , 22nd Jan , 2015

Baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania, vimelaumiwa kwa kubariki njama za kupora ardhi ya wananchi wa Loliondo mkoani Arusha, kwa kutoa habari ambazo zinaficha ukweli kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa eneo hilo na mwekezaji.

Onesmo Olengurumwa (kulia|) akiwa na mmoja wa wakazi wa Liliondo ambao walifanya maandamano yao jijini Dar es Salaam kuelezea hisia zao kuhusu mpango wa kutaka kupora ardhi yao.

Lawama hizo zimetolewa jijini Dar es Salaam leo na Muungano wa Mashirika ya Haki za Binadamu, yanayounda chombo kinachotetea haki ya umiliki wa rasilimali za ardhi na misitu kijulikanacho kama Jukwaa la HakiArdhi Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya wawakilishi wa mashirika mengine, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu - THRDC Bw. Onesmo Olengurumwa, amewasihi wanahabari kusimamia ukweli kuhusu mgogoro huo badala ya kutumika kueneza propaganda kwamba wakazi wa Loliondo sio raia wa Tanzania na kwamba hata mgogoro huo unachochewa na asasi za kiraia kutoka nchi jirani ya Kenya.

Kwa mujibu wa Olengurumwa, wakazi wa Loliondo ni raia halali wa Tanzania ambao wapo eneo hilo tangia enzi ya ukoloni na kwamba propaganda zinazoenezwa kuwa zaidi ya asilimia sabini ya wakazi hao ni wahamiaji kutoka Kenya hazina ukweli wowote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa asasi ya HakiArdhi Bw. Yefred Myenzi amesema iwapo madai kuwa wakazi wa Loliondo ni wahamiaji kutoka Kenya kuna haja ya kuhoji udhaifu wa kiutendaji wa vyombo na mamlaka mbali mbali za serikali kiasi cha kuruhusu raia wa kigeni kuishi nchini kwa kipindi chote cha zaidi ya miaka 20 pasipo kubainika na kuchukuliwa hatua.

Bw. Myenzi amefafanua kuwa taarifa kinzani zinazotolewa kwenye baadhi ya vyombo vya habari ni sehemu ya harakati chafu za mwekezaji za kugeuza ukweli kwa lengo la kudhulumu wananchi ardhi yao anayoitaka kuitumia kwa shughuli za uwindaji.

Mkutano wa leo umehudhuriwa na wananchi kadhaa, madiwani, wawakilishi wa asasi za kiraia pamoja na viongozi wa kimila wa kabila la Wamasai kutoka eneo hilo la Loliondo, ambao kwa gharama zao wamesafiri kuja jijini Dar es Salaam, kueleza ukweli kuhusu mgogoro huo waliodai kuwa mwisho wake ni wao kuondolewa kwenye ardhi yao ya asili walioyoishi toka enzi ya mababu.