Mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro balozi Mwanaidi Maajar.
Mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro balozi Mwanaidi Maajar ametoa mwito huo wakati akizungumza na wajumbe wa baraza la wanawake wenyeji waishio ndani ya hifadhi ya Ngorongoro baada ya kubainika kwa idadi ndogo ya watoto wa kike wa jamii hiyo wanaopata fursa ya elimu.
Baada ya akina mama wa jamii ya wafugaji waishio ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kumweleza Balozi Maajar shauku yao ya kutaka uwiano wa ajira ndani ya mamlaka kuwa asilimia hamsini kwa hamsini, mwenyekiti huyo wa bodi amesema wakati suala hilo likiangaliwa ni vyema akina mama wakachukua jukumu la kuhakikisha kunakuwepo na utashi wa pamoja wa kuwasomesha watoto hususani wa kike, ambao wanaonekana kukosa zaidi haki hiyo.
Awali wanawake hao wa baraza la wafugaji pamoja na mambo mengine wameomba kuboreshwa kwa sekta za Afya kwa kuimarishwa kwa hospitali ya Enduleni na wodi ya akina mama wajawazito, kujengewa uwezo wa namna ya kubadili mila kandamizi zinazoenda kinyume na haki za binadamu.
Wananchi wa jamii ya kifugaji wapatao elfu 85 wanakadiriwa kuishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro eneo pekee linalojumuisha maisha mseto baina ya wanyama na binadamu.