Saturday , 16th Apr , 2022

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameishukuru serikali ya Marekani kwa msaada wa chanjo ya Uviko  - 19 huku akisema zimekuwa msaada mkubwa kwa nchi na kwa watanzania.

Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris ambapo mazungumzo yao yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

“Tanzania tunashukuru kwa msaada wa chanjo za Uviko-19 mlizotusaidia kupitia mpango wa Covax. Ninyi pekee mmetupatia dozi karibu milioni tano ambazo zimekuwa na msaada mkubwa kwetu,” amesema Rais Samia.

Katika hatua nyingine Rais Samia amezungumzia haki za binadamu, utawala wa sheria na demokrasia nchini ambapo amesema Tanzania imeweka mikakati madhubuti katika maeneo hayo.

Amesema Tanzania imechukua hatua za makusudi kuhakikisha kunakuwa na ushirikishwaji, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.