Mashamba ya Miwa wilayani Kilombero
Wakulima wa miwa Kilombero mkoani Morogoro wameilalamikia serikali kushindwa kudhibiti hujuma zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kuingiza sukari kinyemela nchini bila kulipa kodi na kuiweka katika vifungashio vyenye lebo ya Kilombero na kusababisha zaidi ya Tani laki nne za miwa kubaki mashambani bila kuvunwa kutokana na viwanda kushindwa kuuza sukari iliobaki viwandani .
Wakulima hao wametoa malamiko hayo mbele ya kamati ya bunge ya kudumu hesabu za serikali wakati walipotembelea kiwanda cha sukari Kilombero, ambapo wakizungumza kwa uchungu huku wakiwa wameshikilia mifuko ya sukari iliyotoka nchini Uganda na kufungwa upya katika mifuko ya Kilombero wakulima hao wamesema wanapata hasara kwa miwa kuendelea kubaki mashambani na kuomba kamati hiyo iwasaidie kufikisha bungeni malalamiko yao .
Akijibu malalamiko ya wakulima hao mweyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge hesabu za serikali Zitto Kabwe amesema kamati inasubiri taarifa ya TRA kuhusu uingizaji wa sukari nchini kwa kukwepa kodi na mapendekezo ya kamati ni kushauri bunge ili bodi ya sukari iongezewe jukumu la usimamizi kati ya wazalishaji wa sukari na wakulima ili kuhakikisha wakulima wanalipwa kile wanchostahili badala ya wawezekezaji kujinufaisha kupitia migongo ya wakulima.
Nao wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge hesabu za serikai baada ya kusikiliza malalamiko ya wakulima juu ya miwa kubaki mashambani wameshauri wawekezaji wapanue viwanda au kuongeza viwanda vidogo.
Naye mkurugenzi wa bodi ya sukari Henry Semwaza amesema wanahitaji bilioni 11 kulipa fidia wananchi 1554 ili kupisha uwekezaji wa kiwanda kikubwa cha sukari utakafanyka bonde la Ruhipa wilayani Kilombero, yenye ukubwa wa hekta elfu 14 ambao utapunguza tatizo la upungufu wa sukari nchini.