Chama cha Mapinduzi wilaya za Rorya na Musoma mkoani Mara wamemtaka waziri mwenye dhamana na serikali za mtaa kuchukua hatua za haraka kwa wakurugenzi wa halmashauri hizo kabla ya kuitisha maandamano ya kuwatoa katika ofisi zao kwa madai ya kuvuruga zoezi zima la uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Rorya Samwel Kiboye, amesema pamoja na kulalamika kuhusu kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi huo ambao umefanyika Jumapili iliyopita lakini ofisi ya mkurugenzi ilishindwa kurekebisha kasoro hizo hatua ambayo amesema imesababisha uchaguzi huo kuvurugika.
Hata hivyo mwenyekiti huyo ameshauri tume ya taifa ya uchaguzi kufikiria kutumia askari ambao wamepata mafunzo ya jeshi la kujenga taifa kusimamia uchaguzi huo badala ya watendaji wa serikali ambao amedai wengi wao wamekuwa wakitumiwa na vyama vya siasa.
Naye Katibu wa CCM wilaya ya Musoma Jacob Nkomoro, akitoa tathimini ya uchaguzi huo, ameitaka serikali kupitia waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa kuchukua hatua za haraka kumuwajibisha mkurugenzi mtendaji wa manispaa hiyo kwa madai ya kushindwa kusimamia vema uendeshaji wa uchaguzi huo hatua ambayo imefanya taratibu nyingi kukiukwa.