Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Bi Helleni Kijo Bisimba
Makosa ya ukiukwaji wa haki za binadamu hapa nchini yanazidi kuongezeka ambapo kwa kipindi cha miezi sita ya mwaka 2014 zaidi ya watu 700 wameuawa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kishirikina, mauaji ya watu wenye Albinism na watu wanaodaiwa kuwa na hasira kali.
Takwimu hizo zimetolewa na kaimu mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu Bw Ezekiel Masanja wakati wa maadhimisho ya siku ya haki za binadamu duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amesema matukio hayo yanatokana na ukosefu wa elimu juu ya haki za binadamu.
Kufuatia hali hiyo wameishauri serikali elimu ya haki za binadamu kujumuishwa kwenye mfumo wa elimu na itungwe sheria inayolinda haki za mtoa taarifa huku wakitaka wanaotuhumiwa na sakata la Escrow kuwajibika.
Akizungumza katika maadhimisho hayo mwakilishi kutoka mtandao wa jinsia Tanzania TGNP Bi Gema Akilimali amesema ukatili wa kijinsia umekithiri na baadhi ya jamii imeanza kuona ni jambo la kawaida hasa suala la mimba za utotoni na ndoa za utotoni ambazo zimekuwa zikiwaathiri wasichana kisaikolojia kutokana na umri wao na kwamba matukio mengi hayatolewi taarifa kwani yako ndani ya familia.
Kwa upande wa asasi zisizokuwa za kiserikali zilizoshiriki maadhimisho hayo zimesema wakati umefika wanaowanyima haki watu wengine kuwajibishwa hususani wala rushwa katika ofisi za umma na kuongeza kuwa uwajibikaji uanzie ngazi ya juu hadi mtaa na kitongoji huku wakishauri sera ya uwekezaji kuangaliwa upya kwani tafiti zinaonesha kuwa migogoro mingi ya ardhi inatokana na wawekezaji pamoja na kutokuwepo kwa uwiano katika kugawa ardhi kwa wakulima na wafugaji.