Saturday , 6th Dec , 2014

Nafasi ya vijana kujiajiri kupitia elimu ya ufundi stadi nchini huenda ikawa na nafasi kubwa na kusaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira, baada ya mamlaka ya vyuo vya elimu ya ufundi stadi nchini VETA, kukusudia kuboresha shughuli za mafunzo

Mkurugenzi wa VETA nchini Zebedayo Moshi.

Mkuu wa Veta nchini, Mhandisi Zebedayo Moshi, amesema hayo wakati akizungumza na wanajumuiya wa elimu ya ufundi stadi mkoani Morogoro, ambapo amesema wanakusudia kukiingiza chuo hicho katika utafiti wa masuala ya ufundi stadi, kuwa na walimu wenye uwezo wa kutunga mitaala itakayotumika kwenye vyuo vyote vya ufundi stadi na kuanza kutoa mafunzo ya uongozi katika elimu ya ufundi stadi.

Kwa Upande wake Mkuu wa mafunzo katika chuo hicho, Auforo Maro, akibainisha jitihada mbalimbali zilizoanza kufanywa kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa, ikiwemo kuanzisha mfumo wa elimu ya masafa kabla ya kumalizika kwa mwaka 2015.

Naye Mkuu wa wilaya ya Morogoro Said Amanzi amevitaka vyuo vya ufundi stadi kubuni mitaala ya kuongeza ubora wa bidhaa ili ziwe na thamani na kukuza soko la mazao yanayozalishwa, ikizingatiwa wengi wa wakulima wamekuwa wakiuza bidhaa ghafi ambazo hazijasindikwa wala kuboreshwa,

Aidha Mkuu wa Chuo Cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro, MVTTC, Stephen Lazaro amebainisha wameanza kuangalia upya mfumo wake wa utendaji ili kukidhi mahitaji kuendeleza watumishi sambamba na kuongeza uwezo wa chuo hicho kutoa mafunzo katika nyanja mbalimbali za elimu zenye kuhitajika katika soko.

Tanzania ina takribani vyuo 720 vya ufundi stadi vikiwemo 27 vinavyomilikiwa na VETA na vingine vikimilikiwa na serikali na taasisi za dini na vinahitaji walimu 3028 hivyo kuwa na pengo la walimu 2,700 katika vyuo vya ufundi stadi.