Monday , 16th May , 2016

Kikosi cha timu ya Taifa ya Viajana cha Tanzania Serengeti Boys leo kitatupa tena karata yake ya pili kwa wenyeji timu ya vijana ya India katika michuano ya kirafiki ya vijana Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa nchini India.

Afisa habari wa Shirikisho la Soka nchini TFF Alfredy Lucas amezungumza kwa niaba ya kocha wa kikosi hicho Bakari Shime ambaye amewasiliana naye ambapo amesema, kikosi kipo vizuri kwa ajili ya mchezo huo wa leo.

Lucas amesema, michuano hiyo inachukuliwa kwa uzito mkubwa na mchezo wa leo wataibuka na ushindi mara baada ya mchezo wa awali uliopigwa hapo juzi Serengeti Boys kuweza kutoka sare ya bao 1-1 na timu ya Taifa ya vijana ya Marekani.

Baada ya mchezo wa leo Serengeti itashuka tena dimbani Mei 19 kumenyana na Korea Kusini kuanzia Saa 7:30 mchana kwa saa za India.

Kikosi hicho cha wachezaji 22 cha Serengeti chini ya Kocha Bakari Shime kipo mjini humo kwa ajili ya mashindano hayo, yatakayofikia tamati Mei 25, mwaka huu.

Kikosi hicho ni makipa; Ramadhan Kabwili, Kelvin Kayego na Samwel Brazio wakati mabeki wa pembeni ni Kibwana Shomari, Nicson Kibabage, Israel Mwenda na Ally Msengi.

Mabeki wa kati ni Issa Makamba, Nickson Job na Ally Ng'anzi huku viungo wakiwa ni Maulid Lembe, Asad Juma, Kelvin Naftari, Yasin Mohamed na Syprian Mwetesigwa na washambuliaji ni Aman Maziku, Rashid Chambo, Enrick Nkosi, Yohana Mkomola, Mohamed Abdallah, Shaban Ada na Muhsin Mkame.