Sunday , 30th May , 2021

Klabu ya soka ya Chelsea ya Uingereza imeshinda ubingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, baada ya kuifunga Manchester City 1-0 usiku wa kuamkia Mei 30, 2021. Goli pekee la Chelsea lilifungwa na Kai Havertz dakika ya 42.

Chelsea wakishangilia ubingwa

Huu ni ubingwa wao wa pili katika historia ya klabu hiyo ambapo ubingwa wa kwanza walitwaa mwaka 2012 kwa kuwafunga Bayern Munich.

Rekodi mbalimbali zilizowekwa

Mlinzi wa kati wa Chelsea raia wa Brazil Thiago Silva ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa tano kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu miwili mfululizo akiwa na klabu tofauti wengine Marcel Desailly, Paulo Sousa, Samuel Eto’o na Álvaro Morata.

Mlinzi wa kati wa Chelsea Thiago Silva

Thiago Silva pia ndio mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi (miaka 36) kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ndani ya kikosi cha Chelsea akiivunja rekodi ya Claude Makélélé dhidi ya Manchester United mwaka 2008 alipocheza akiwa na miaka 35 na siku 93.

Kocha Pep Guardiola amepoteza fainali mbili za mashindano katika historia yake ya kufundisha soka tangu mwaka 2008. Alipoteza fainali ya Copa del Rey msimu wa 2010-11 akiwa na Barcelona na sasa amepoteza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Chelsea.

Kocha wa Man City  Pep Guardiola

Wakati kocha wa Chelsea Thomas Tuchel ametwaa ubingwa katika fainali yake ya pili baada ya kupoteza fainali ya msimu uliopita 2019-20 dhidi ya Bayern akiwa na PSG.

Kocha wa Chelsea Thomas Tuchel

Pia Thomas Tuchel amekuwa kocha wa pili kumfunga Pep Guardiola katika mechi tatu mfululizo za mashindano yote akitanguliwa na kocha wa Liverpool Jürgen Klopp ambaye alifanya hivyo mwaka 2018.