Wednesday , 5th May , 2021

Leo Domokaya ametambulisha nyimbo zake mbili "My chick" na "I care" kupitia PlanetBongo ya East Africa Radio huku amebeba barua kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambayo ameishikilia mtangazaji Dullah Planet hapo kwenye picha.

Msanii Domokaya akiwa kati pichani, kulia ni Mtangazaji Dullah Planet akiishika barua hiyo

Barua hiyo ni kibali kutoka BASATA ambacho kinathibitisha nyimbo hizo zinafaa kusikilizwa na watu wa umri wote.

Domokaya ni moja kati ya wasanii wachache waliofuata taratibu hizi mpya za BASATA ambazo zimeonekana kupingwa na wasanii wengi tangu zilipotangazwa.

Akizungumzia kuhusu utaratibu huo mpya wa BASATA Domokaya ameeleza kuwa "Siwezi kusema moja kwa moja kama ni sawa au sio sawa, hii sheria ndio imeanza kufanya kazi sasa hivi, tungetoa sauti mwanzo kabla ya kutibu kipele, tangu tulipopewa onyo la kuacha kuimba hayo matusi tungeachana nayo tangu zamani

"Mimi pia nimewahi kurudishwa na wimbo wangu lakini tayari nishajifunza, nilifuata hizi taratibu mapema nilijua kuwa nakuja kutoa nyimbo zingine japo mfumo unakwamisha kwa namna moja au nyingine" ameongeza