Saturday , 1st May , 2021

Afisa Habari na mawasiliano wa klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli amesema uongozi wa klabu hiyo utamfungulia mashitaka nahodha wa klabu ya TZ Prisons, Benjamin Asukile kwa kutoa tuhuma nzito akidai baadhi ya watu wa Yanga walitaka kutoka rushwa ili kununua mchezo wao.

Msemaji wa klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli (kushoto) akiwa na Mkuu wa uwekezaji wa GSM kwenye klabu hiyo, Eng.Hersi Said (kulia).

Bumbuli ametoa maelezo hayo asubuhi ya leo kupitia ukurasa wake wa Instagram na kusisitiza kuwa watapeleka tuhuma hizo kwenye vyombo husika ili Asukile atoa ushahidi maana Yanga haipo tayari kuchafuliwa kwa tuhuma nzito kama hizo.

Baada ya mchezo wa jioni ya jana kumalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya TZ Prisons kwenye dimba la Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa na kutinga robo fainali ya kombe la Shirikisho nchini, Asukile alitoa tuhuma hizo akiamini wamehujumiwa.

Asukile alisema, “Sisi hatujakwama popote ila tumeshindwa kucheza kwa kuwa wenyewe walikuwa wametuzidi kwa kuwa wamemuongeza refa uwanjani, kwa hiyo kama umemuongeza refa uwanjani sisi hatuwezi kumshinda refa, ila kwa wachezaji sisi tuliwazidi”.

(Nahodha na mlinzi wa kushoto wa klabu ya TZ Prisons, Benjamin Asukile.)

Maneno hayo ya Asukile ambayo aliyatoa akiwa na jazba kubwa yalikuja baada ya mlinzi wa Yanga, Lamine Moro kumundondosha mshambuliaji wa TZ Prisons, Jeremia Juma kwenye eneo la hatari akiamini ilipaswa kuwa penalti na kuwa kwenye nafasi nzuri ya kusawazisha bao lakini haikuwa hivyo.

Asukile akaendelea na kusema, “Refa ametunyima penati, tukimuuliza kwa nini hajapuliza filimbi anasema hajaona. Sasa kwa nini TFF wanatupangia marefa vipofu ambao hawaoni?”

Baada ya hapo ndipo akatoa tuhuma zenye tafsiri ya baadhi ya watu kutoka klabu ya Yanga waliwafuata kutaka kuwapa rushwa ili kununua mchezo huo jambo ambalo bumbuli amelitaka litolewe ushahidi.

“Hawa wamekuja wanapiga simu muda wote wanaeatafuta watu walete hela Milioni 40” Asukile akamalizia.

Katika kujibia tuhuma hizo bumbuli ameandika kuwa, 

“Nahodha wa Tanzania Prisons Benjamin Asukile ametoa tuhuma mzito dhidi ya Yanga, 1. Amesema tuliwazidi kwa sababu tulimuongeza Refa upande wetu, Hili tunataka alithibitishe, Kivipi na kwa namna gani!?
2. Walikuwa wakiwapigia simu na kutaka kutoa Mil 40 (Rushwa) I'll watuachie game, hili pia tunataka alithibishe mbele ya ya Mamlaka husika.

Hakuna namna ambayo Yanga tunaweza kuvumilia kuchafuliwa kwa kiwango hiki, sasa huo ujasili wa Asukile na kujitoa ufahamu kuona wao ni wababe ameutoa wapi? Tutazifikisha tuhuma hizi zote kwa Mamlaka husika ASAP”.