Friday , 30th Apr , 2021

Klabu ya soka ya Yanga imetinga hatua ya robo fainali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports Federation Cup baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya waliokuwa wenyeji wao maafande wa Tanzania Prisons.

Kikosi cha Yanga kilichocheza leo na Tanzania Prisons na kufanikiwa kutinga robo fainali ya kombe la shirikisho.

Bao pekee la wanajangwani jioni ya leo lilisukumiziwa kimiani na mshambuliaji Yacouba Sogne dakika ya 54 ya mchezo akimalizia kazi nzuri ya Saido Ntibazonkiza aliyetoa pasi maridhawa ambayo bila ya ajizi mfungaji akaweka mpira kimiani na kumuacha mlinda mlango wa Tanzania Prisons Jeremia Kisubi asijue cha kufanya.

Mchezo wa mapema hii leo ulizikutanisha Mwadui ambayo iliibuka na ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwa bao 2-0 na kutinga robo fainali ambapo mabao ya washindi yalifungwa na Roshwa Radhid dakika ya 14 na Wallace Kiango dakika ya 24 ya mchezo.

Yanga na Mwadui zinaungana na vilabu vya Rhino Rangers, Azam Fc, na Biashara Mara United ambazo juzi na jana zilishinda katika michezo yao waliyoicheza.

Hatua ya robo fainali ya michuano hiyo  itaendelea  kesho kwa michezo miwili ambapo Dodoma Jiji watachuana dhidi ya KMC wakati wekundu wa msimbazi Simba ambao ndio mabingwa watetezi watakipiga dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam.

Hatua ya 16 bora itamalizika Mei 2 mwaka huu ambapo Jkt Tanzania itaumana na Namungo kutoka Mkoani Lindi.