Sunday , 25th Apr , 2021

Tanzania inauwezo wa kupata hitaji lake la mafuta ya kula ambayo yanahitajika nchini kwa mwaka mzima kiasi cha lita tani 570,000-600,000 kwa kutumia mbegu za mazao zinazozalishwa kwa wingi hapa nchini.

Mafuta ya Alizeti na Mbegu za Alizeti

Akizungumza na EATV Ringo Iringo ambaye ni msindikaji wa mbegu ili kupata mafuta amesema yapo mafuta yanayotokana na mbegu, samaki na kutoka kwa wanyama, ingawa mafuta mengi yanatokana na mbegu za mazao.

''Tanzania tunaongoza kwa kuzalisha mbegu za mafuta barani Afrika ambapo mbegu hizo za mimea ni pamoja na Alizeti, Michikichi, Korosho, Karanga, Mahindi, Mchele, Karanga, Nazi,Ufuta, maboga na matikiti,'' amesema Ringo Iringo Msindikaji wa mbegu za mafuta.

                         Bw. Ringo Iringo -Msindikaji Mbegu za Mafuta
Ameongeza kuwa viwanda vya kusindika mbegu kutoa mafuta vipo vingi na vina uwezo, changamoto kubwa ni ubora wa mbegu, mfano mzuri ni katika mbegu za Alizeti, Tanzania ni ya kwanza katika uzalishaji na Afrika Kusini ni ya pili ila inaongoza kutoa mafuta mengi ya zao hili kuliko Tanzania.

''Afrika ya Kusini inazalisha tani laki nane na nusu hadi laki tisa za mbegu za zao la Alizeti kwa mwaka na kuzalisha tani laki 7 za mafuta huku Tanzania ikizalisha mbegu za Alizeti tani milioni 2.5 hadi 3 na kuzalisha tani laki 2 za mafuta ya Alizeti kwa mwaka” amesema Ringo Iringo Msindikaji wa mbegu za mafuta

Aidha, Bwana Iringo amesema mwaka jana mvua zilikuwa nyingi ziliharibu mazao shambani hasa zao la Alizeti ambalo hutoa asilimia 80 ya mafuta yote ya kula yanayosindikwa hapa nchini,hii ni moja ya chnangamoto ya mafuta ya kula kwa sasa.

Ameongeza pamoja na changamoto hiyo lipo suala la kubadilisha ili tujitosheleze na mafuta ya kula kwa serikali kuziwezesha taasisi zinazozalisha mbegu ili wakulima wazipate na kutosheleza kote nchini.

''Wakulima wanahitaji mbegu tani elfu 5 za Alizeti kwa mwaka huu, lakini uwezo wa nchini kutoka Wakala wa kuzalisha mbegu (ASA) na watafiti wa mbegu za mafuta ya Ilonga zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo ni tani 350 hadi 400 hivyo tuko chini na haitoshelezi hitaji la wakulima, “amesema Ringo Iringo Msindikaji wa mbegu za mafuta

Bw. Iringo amesema mwezi wa Februari mwaka huu vyama vya usindikaji mafuta Tanzania walikutana na Wizara ya Kilimo ili kuona kama haiwezekani kuwezesha taasisi za kuzalisha mbegu za ASA na Ilonga, kuongezewa fedha maana wana mashamba makubwa, basi ishirikishe sekta binafsi katika uzalishaji wa mbegu.

Kwa upande mwingine , Bw. Iringo amesema kwa sasa hapa nchini mahitaji ya mafuta ni mengi kwa kuwa wajasiriamali wamekua wengi, na pia janga la corona nchi nyingi ziko katika 'lockdown' zikiwemo za Jumuiya ya SADC na Afrika Mashariki hivyo sisi tungeweza kuzalisha mafuta ya kula kwa wingi na kuyauza.

  Mh.Samia Suluhu Hassan -Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Akihutubia Bunge April 22,2021.

Akilihutubia Bunge jijini Dodoma April 22 wiki hii,Rais Samia Suluhu Hassani alisema serikali yake itainua sekta ya kilimo kwa kuhakikisha kuna upatikanaji wa wataalamu,mbegu na mbolea kwa wakulima kwa kuwa sekta hii imeajiri watanzania kwa Asilimia 65.