Kiungo matata wa Yanga, Haruna Niyonzima(Wa mbele kabisa pichani) alipokuwa mazoezini katika kikosi cha msimu uliopita.
Kocha mkuu wa Yanga, Cedric Kaze amesema Niyonzima anasumbuliwa na ugonjwa wa Malaria hivyo hakujumuika na wenzake katika mazoezi ya matayarisho ya mchezo huo utakaopigwa Novemba mosi mwaka huu huko mjini Musoma.
Akizungumzia kuhusu hali za wachezaji Kaze amesema''Maandalizi mazuri na tumepata sehemu nzuri ya mazoezi, wachezaji wote kwa asilimia kubwa wanaendelea vyema kasoro Haruna Niyonzima ambaye anaumwa Malaria.
Yote kwa yote timu inabidi icheze ili ipate ushindi bila kisingizio chochote, tupo imara na tunasubiri mchezo dhidi ya Biashara ili tuone namna ambavyo tunaweza kuonesha tulichonacho.''
Yanga ni timu pekee katika ligi kuu ya Tanzania bara ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja, ikiwa imeshinda mara sita na sare moja.
Kwa upande wa Biashara wanajivunia rekodi nzuri katika uwanja wao wa nyumbani dhidi ya Yanga kwakuwa waliwafunga mara moja na sare katika mechi mbili walizocheza nao.
Vilevile Biashara haijapoteza mchezo hata mmoja katika Uwanja wake wa nyumbani msimu huu, na wapo katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 16 katika mechi 8 walizoshuka dimbani.