
Kushoto ni RPC Arusha ACP Salum Hamduni na kulia ni mgombea ubunge jimbo la Arusha mjini Godbless Lema.
Taarifa hiyo imetolewa hii leo Oktoba 6, 2020, na Kamanda wa polisi mkoani humo ACP Salum Hamduni,imesema kuwa awali taarifa zilienezwa kwamba wamekamatwa na watu wasiojulikana jambo ambalo si la kweli, kwani maaskari wote waliofika kwenye ofisi hizo walikuwa na sare.
"Jana Oktoba 5 jeshi la polisi lilipokea taarifa fiche kwamba kwenye ofisi binafsi za Godbless Lema, kuna watu ambao wamekuwa na kawaida ya kukusanyika pale kuendesha mafunzo yenye lengo la kutenda uhalifu wa kijinai ya kuingilia mifumo ya mawasiliano ya kibenki, mara baada ya taarifa hizo kupokelewa wapelelezi walifika eneo hilo ili kujiridhisha na taarifa hizo na taratibu zote zilifuatwa", amesema ACP Hamduni.
"Kumekuwa na taarifa ambazo zinazagaa kwenye mitandao ya kijamiii kwamba watu wasiofahamika wamevamia, hapana ni jeshi la polisi na askari waliofika pale walikuwa wamevaa sare na askari wapelelezi wote walikwenda kwa pamoja kwa nia ya kufanya upekuzi na kuwakamata watu wote waliokuwa wakihusishwa na tuhuma hizo na jumla ya watu watano walikamatwa" ameongeza ACP Hamduni.
Waliokamatwa na ambao wanashikiliwa na jeshi hilo mpaka sasa ni Viola Likindikoki, Wilbert Tarimo, Nelson Lema, Joshua Lukumay na Mohamed Degera na jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi na ushahidi ukipatikana hatua zaidi zitafuata.