Wednesday , 30th Sep , 2020

Serena Williams ajiondoa michuano ya Ufaransa. Bingwa mara tatu, Serena Williams amejitoa katika mashindano ya Ufaransa kutokana na majareha ya kisigino.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 39, alitazamia kucheza mechi yake ya raundi ya pili dhidi ya Mbulgaria Tsvetana Pironkova siku ya jumatano.

Raia huyo wa Marekani mwenye mataji 23 ya grand slam kwa alikua na malengo ya kuifikia rekodi ya Margaret Court ya mataji 24 

Williams, alipata majeraha ya kisigino katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya wazi ya Marekani kwenye ushindi dhidi ya Victoria Azarenka mapema mwezi huu. “Ninafikili ninahitaji wiki nne mpaka sita, ya kukaa bila kufanya kazi yoyote ngumu.

Aliwaambia waandishi wa habari. Nimekua nikihangaika kutembea hiyo ni dalili mbaya ninahitaji kujiweka sawa”. Williams, alitwaa French Open mwaka 2002,2013 na 2015 na anashikilia nafasi ya tisa kwa ubora duniani.

HII INAMAANA GANI KWA SERENA? 

Kuifikia rekodi ya mataji 24 ya grand Slam, ni ndoto ngumu kutimia kwa Serena Williams kulingana na umri wake kwa sasa wa miaka 39, mbaya zaidi majeraha anayoyapata mara kwa mara yanaongeza changamoto dhidi ya malengo yake.

Serena hatoonekana tena katika mashindano makubwa ya tenesi kwa mwaka huu, mpaka katika ratiba mpya za kimashindano za mwaka ujao kutokana na majeraha yake ya kisigino.

Majeraha ya kisigino, aliyoyapata katika jiji la New York hayakupata muda wa kutosha wa kupona .

Baada ya kufika hatua ya nusu fainali katika mashindano ya wazi ya Marekani, aliunganisha kucheza mashindano ya wazi ya Ufaransa bila kupumzika inaweza ikawa ni sababu ya kutonesha majeraha yake.

Ni ngumu kushinda Grand Slam akiwa na majeraha yanayojirudia mara kwa mara na umri wake kuonyesha dalili za kuanza kumsaliti, majeraha ya goti na mgongo yamekua kikwazo kikubwa sana kwake kushindana kwa asilimia mia moja.