Monday , 24th Aug , 2020

Ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani kilichopo mbezi Luis jijini Dar es salaam umejatwa kufikia asilimia 77 kabla ya kukamilika kwake Oktoba mwaka huu.

Muonekano wa sehemu ya majengo katika stendi ya mabasi yaendayo mikoani Mbezi Luis

Akizungumza na EATV leo mhandisi na msimamizi wa ujenzi huo kutoka halmashauri ya jiji la Dar es salaam Allex Masatu amesema hadi kufikia tarehe 15 mwezi wa kumi kituo hicho kitakuwa tayari kimekamilika kama mkataba unavyowaelekeza, kutokana na ujenzi unaoendelea kulingana na ramani ya mradi huo.

“Hadi kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho zaidi ya shilingi bilioni 50 zitakuwa zimetumika kama gharama za ujenzi”alisema Masatu

Ameongeza kuwa uwekezaji huo unaofadhiliwa na fedha za ndani utasaidia kuboresha huduma za usafiri nchini pamoja na kuongeza uwekezaji kupitia biashara baada ya kuwepo kwa maeneo yaliyotengwa mahsusi kwa watoa huduma na wafanyabiashara wa ngazi zote.