Serikali ya wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera imeimarisha ulinzi katika maeneo ya mipaka ya nchi, kuunda kamati Tano za ufuatiliaji ikiwemo uelimishaji, ukaguzi na usambazaji wa vifaa vya kunawa mikono katika mipaka ya nchi kwa lengo la kudhibiti ugonjwa hatari wa Ebola usiwakumbe wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya mipakani mwa nchi.
Hatua hii inakuja baada ya kubainika kuwa mtu mmoja amepoteza maisha nchi jirani ya Uganda maeneo ya Mbalala karibu na mpaka wa Tanzania, kwa ugonjwa wenye dalili sawa na Ebola.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kyerwa kanali mstaafu Benedicti Kitenga na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa Bw. George Mshindo wamesema kuwa serikali imelazimika kuimarisha ulinzi katika maeneo ya mipaka ya nchi ili kuepusha wananchi wasiambukizwe ugonjwa hatari wa Ebola na kwamba kamati zilizoundwa zimetakiwa kufanya kazi usiku na mchana.
Kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya ya Kyerwa Dr. Mohamed Mpunjo amesema kati ya watoto 170,000 waliotarajiwa kupatiwa chanjo ya Surua na Rubela katika wilaya ya Kyerwa wanafunzi 7791 wa shule za msingi na sekondari hawakupatiwa chanjo baada ya kubainika ni wahamiaji haramu waliokuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria za nchi ambapo serikali imewarejesha makwao.