Saturday , 25th Oct , 2014

Wachezaji zaidi ya 60 toka vilabu vya mchezo wa Darts jijini Dar es salaam hii leo wameonyeshana umwamba katika michuano ya klabu bingwa ya mkoa inayoandaliwa na klabu ya darts ya Lugalo

Baadhi ya washiriki wa michuano ya Lugalo wakichuana katika michuano hiyo.

Mashindano ya klabu bingwa ya mkoa wa Dar es salaam mchezo wa vishale [Darts] yajulikanayo kama Ngome Flutin Cup yameanza hii leo katika ukumbi wa jeshi Lugalo Msasani Beach Club yakishirikisha klabu mbalimbali

Mratibu wa shindano hilo ambalo mara hii ni ya tatu kufanyika Kamdas Kibago amesema shindano hilo ni la kila mwaka na linashirikisha vilabu vya wanaume na wanawake ambavyo vinachuana kwa mtindo wa ligi.

Kibago amesema lengo kubwa la kuandaa michuano hiyo kwa mkoa wa Dar es salaam ni kuwaweka pamoja wachezaji na kujenga umoja miongoni mwa vilabu na pia kukuza vipaji kwa wachezaji wa mkoa huo

Kwa upande mwingine katibu mkuu wa chama cha mchezo wa darts mkoa wa Dar es salaam Bi Subira Waziri amesema mchezo huo una changamoto kubwa hasa kwa watoto na wanawake kutokana na mazingira yanayochezewa mchezo huo kuwa ni sehemu za vileo.

Subira amesema ni vigumu kuwapata watoto katika mchezo huo na hata wanawake wamekuwa ni wachache yote kutokana na mchezo huo kuchezwa katika maeneo yanapouzwa vileo kitu ambacho wengi wanakitafsiri kuwa mchezo huo huchezwa na walevi.

Aidha Subira amewataka watanzania kuachana na fikra hizo kuwa mchezo huo huchezwa na walevi kutokana na kucheza maeneo ya bar kwa kuwa mchezo huo pamoja na kuchezwa maeneo hayo kutokana na kukosekana viwanja ama kumbi maalumu za mchezo huo basi isitafsiriwe hivyo

Akimalizia Subira amesema yeye akiwa ni katibu mkuu mwanamke atahakikisha anatoa elimu na anahamasisha wanawake kujitokeza katika kucheza mchezo huo kwani nao ni mchezo kama michezo mingine na unatambulika kidunia na watu wanapata fedha kutokana na mchezo huo.