Wednesday , 22nd Jul , 2020

Pamoja na kupata ushindi dhidi ya Arsenal Jumanne hii, na kutoka eneo la kushuka daraja, bado Aston Villa itahitaji kushinda mchezo wa mwisho uliobaki.

Mshambuliaji wa Aston Villa na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akifunga bao dhidi ya AFC Bournemouth katika mchezo wa EPL.

 

Villa ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Washika mitutu Arsenal, kwa bao la Mmisri Trezeguet baada ya mpira wa kona kudondokea miguuni kwake na kuachia shuti kali lililompita mlinda mlango wa Arsenal Emiliano Martinez.

Ushindi huo unaifanya Villa kutoka eneo la kushuka daraja na kupanda hadi nafasi ya 17 kwa kufikisha alama 34 huku mchezo mmoja ukiwa umebaki.

VITA YA MTU TATU
Aston Villa inalingana pointi na Watford hivyo inahitaji kushinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya West Ham Jumapili hii, huku ikiiombea Watford ipoteze mchezo wake dhidi ya Arsenal.

Villa inabebwa kudaiwa idadi ndogo ya magoli kuliko Watford, ambapo ina 26 dhidi ya 27 ya wapinzani wake.

Bournemouth iliyopo nafasi ya 19 ikiwa na alama 31 nayo inaweza kujinasua kutoka nafasi hiyo hadi eneo la 17 endapo itashinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya Everton, huku ikiombea Aston Villa na Watford wapoteze michezo yao.

Hii inamaana kwamba Bournemouth atafikisha alama 34 kama walizo nazo washindani wake, na kitakacho amuliwa ni idadi ya mabao wanayotofautiana lakini itategemea na matokeo ya washindani wake ambao ni Watford na Villa.

TAKWIMU
Villa imeshinda mabao 6 tangu kurejea kwa ligi na kati ya hayo Trezeguet amefunga mabao matatu.

Katika mechi 3 zilizopita Aston Villa imeshinda mechi mbili na kupata sare moja hivyo kujikusanyia alama 7.

 

Ushindi wa jana dhidi ya Arsenal ni wa kwanza tangu Disemba ya mwaka 1998.

JE SAMATTA ATAUZWA?

Aston Villa ni timu anayocheza Mtanzania Mbwana Samatta akijiunga nayo mwezi Januari mwaka huu akitokea Genk ya Ubelgiji, lakini amekuwa katika wakati mgumu wa kutofunga mara kwa mara kutokana na muda mfupi aliotua klabuni hapo.

Samatta ambaye ni Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars amefunga goli 1 tu katika mechi 13 za Aston Villa.

Kuuzwa si rahisi kutokana na mkataba wake bado una miaka 4 mbele lakini inawezekana akapewa muda zaidi wa kuangaliwa endapo Villa itabaki kwenye EPL msimu ujao.