Mgombea Urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi
Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Julai 19, 2020 wakati akizungumza na wananchi wa Pemba baada ya kutambulishwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein, amesema kuwa yuko tayari kuupigania Muungano na wananchi wasidanganyike na wagombea wenye matabaka.
“Tusilete mgawanyiko sote ni Wazanzibar hakuna Mpemba wala Muunguja hapa, asije yeyote kuwavuruga. Niko tayari kwa mapambano wao waje tu, aje yeyote”, amesema Dkt. Mwinyi
Ameongeza kuwa, "Nimekaa Wizara ya Ulinzi muda mrefu, mambo yangu mimi nafanya kijeshi sifanyi hadharani ndiyo maana hamjawahi nisikia kwenye vyombo vya habari nikimfokea mtu yeyote. Ila katika uongozi wangu wasiowaadilifu watanielewa mapema”.
Kwa Upande wake Rais wa Zanzibar Dkt. Shein akizungumza mara baada ya kumtambulisha mgombea huyo amewaonya wagombea wa nafasi ndani ya chama chake na wapinzani kutotumia lugha za kudharirisha majukwaani.
“Tusitumie lugha mbaya majukwaani wakati wa kampeni, tuheshimiane tumwage sera na lazima CCM Zanzibar ishinde kila ngazi, Wazanzibar wanakipenda Chama chao na wanakiamini sana", amesema Dkt. Shein.