Sunday , 19th Jul , 2020

Aliyewahi kuwa waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe, leo Julai 19, 2020 amerejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya ACT Wazalendo.

Bernard Membe akirejesha fomu

Makabidhiano hayo yamefanyika Ofisi ya ACT Wazalendo Magomeni, jijini Dar es salaam ambapo amekabidhi fomu hizo kwa Naibu Katibu Mkuu Bara wa ACT Wazalendo Ndugu Joran Bashange.

Membe ambaye kauli mbiu yake alitaja kuwa ni Kazi na Bata, alikubali kuwania nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ACT Wazalendo, kwa kile alichodai kwamba huo ni wakati muafaka kwake wa kushiriki mazungumzo na vyama vingine ili waweze kusimamisha mgombea mmoja.

Julai 16 wakati akizungumza na wanachama wa ACT Wazalendo, alieleza ni kwa namna gani alifedheheshwa, baada ya kufukuzwa uanachama na CCM, "Mimi nimefukuzwa tena kwa aibu na kutukanwa na vijana ambao ningeweza kuwazaa, na sikutenda kosa lolote hata mbele ya Mungu, kosa nililofanya ni la kugombea Urais 2015".