Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali, John Mbungo.
Hayo yameelezwa na Brigedia Jenerali, John Mbungo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, wakati anafungua warsha ya wadau wa uchaguzi, kujadili namna ya kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, jijini Dar es Salaam.
Brigedia Mbungo ameeleza kuwa, gharama za uendeshaji uchaguzi ndio chanzo cha vitendo vya rushwa, ambapo baadhi ya wafanyabiashara hutumia mwanya huo, kujinufaisha baada ya wagombea waliowafadhili, kupata uongozi Serikalini.
"Mara nyingi chanzo kikuu cha rushwa katika uchaguzi ni gharama za uchaguzi, jambo hili husababisha wagombea au watia nia kutumia ushawishi pamoja na nguvu ya fedha ili kurubuni wapiga kura wawachague, mgombea au wagombea wenye uwezo wa kifedha, hutumia kigezo hicho cha fedha kuwarubuni wananchi ili wawachague," amesema Brigedia Mbungo.
Kuhusu warsha hiyo, Brigedia Mbungo amesema TAKUKURU imeamua kukutana na wadau wa uchaguzi, ili kuunga mkono azma ya Rais John Magufuli, ya kutaka uchaguzi huo unafanyika kwa haki, huru na usawa.
Warsha hiyo imehudhuriwa na Viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa Dini, Msajili wa Vyama vya siasa pamoja na Tume ya Uchaguzi.



