Friday , 3rd Jul , 2020

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga, inamshikilia Joseph Jonas Tasia kwa kukutwa na doti 600 za vitenge vyenye nembo za Chama Cha Mapinduzi na vingine vya kawaida. 

Mfano wa vitenge vyenye nembo ya CCM

Taarifa ya TAKUKURU leo Julai 3, 2020 imeeleza kuwa Joseph alikamatwa Juni 29, 2020 Saa 3:00 Usiku nyumbani kwake mtaa wa Mwasele B.

Taarifa imefafanua kuwa mtuhumiwa huyo ni mfanyabiashara wa usafiri wa magari madogo maarufu kama TAXI na hana duka wala hafanyi biashara ya nguo.

TAKUKURU wameongeza kuwa jambo la yeye kuwa na vitenge hivyo nyumbani kwake linaashiria kuwa vilikuwa vinaandaliwa kwaajili ya kutumika katika kufanya ushawishi kwa wapiga kura.

Aidha TAKUKURU mkoani Shinyanga imewaonya wote wenye nia ya kutumia taarifa zozote ambazo inazifanyia uchunguzi kwa lengo la kujinufaisha kwani kwa kufanya hivyo ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.