Monday , 13th Oct , 2014

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dk. Mohammed Gharib Bilal amewaongoza maspika wa mabunge ya Jumuiya ya madola kanda ya Afrika, mawaziri, wabunge na wananchi wa mkoa wa Mwanza katika mazishi ya Dkt William Shija.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dk. Mohammed Gharib Bilal amewaongoza maspika wa mabunge ya Jumuiya ya madola kanda ya Afrika, mawaziri, wabunge na wananchi wa mkoa wa Mwanza katika mazishi ya aliyekuwa katibu mkuu wa mabunge ya jumuiya hiyo Dk. William Shija katika kijiji cha Nyampande wilayani Sengerema.

Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal ambaye aliwahi kufanya kazi pamoja na Dk. William Shija kama katibu mkuu wa wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya juu kwa miaka 10 amesema kuwa marehemu Dk. William Shija alikuwa mchapakazi hodari, mwenye bidii, mwadilifu na aliyependa watu, hivyo kifo chake ni pigo kubwa siyo tu kwa watanzania bali katika jumuiya ya kimataifa ambako amehudumu kama mtu wa kwanza mweusi kuwa katibu mkuu wa mabunge ya jumuiya ya madola tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo mwaka 1911.

Kwa upande wake spika wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Anne Makinda amesema upinzani sio uadui, na kuwataka wanasiasa kuiga mfano wa maisha ya Dk. William Shija ya uadilifu na kutojilimbikizia mali huku mwakilishi wa bunge la Kenya Seneta Moses Watangula akisema kwamba umoja wa mabunge ya jumuiya ya madola umeondokewa na mtu shujaa ambaye alisimama imara kupinga kila aina ya ubaguzi uliokuwa ukifanywa na wazungu dhidi ya waafrika.

Mtoto wa marehemu Dk. Shija, Anna- Claire Shija amesema familia hiyo daima itaendelea kumuenzi marehemu baba yao kwa matendo mema, ambapo Padri Revocatus Makonge wa parokia ya Nyampande akihubiri katika ibada ya misa ya mazishi iliyoongozwa na askofu wa kanisa katoliki jimbo la Bunda ambaye pia ni msimamizi wa kitume wa jimbo la Geita mhashamu Renatus Nkwande.

marehemu Dk. William Shija ambaye alizaliwa mwaka 1947 wilayani Sengerema ameacha mjane na watoto watano.