Thursday , 16th Apr , 2020

Afisa Mhamasishaji na Msemaji wa klabu ya Yanga, Antonio Nugaz ametaja njia inayotumika na kocha wa klabu hiyo, Luc Eymael katika kutoa mpangilio wa mazoezi pamoja na ufuatiliaji wa wachezaji katika kipindi hiki cha janga la Corona.

Afisa Mhamasishaji na Msemaji wa Yanga, Antonio Nugaz

Hiyo ni baada ya ligi kusimama katika kipindi hiki ambacho janga la Corona linaendelea kusambaa duniani, ambapo 'program' za mazoezi zinafanyika nyumbani kuepuka mikusanyiko ya wachezaji kwa pamoja.

Akizungumzia kuhusu njia za kutoa mazoezi inayotolewa na kocha Eymael, Antonio Nugaz amesema, "kila mmoja anafanya mazoezi akiwa nyumbani na lengo ni kutii agizo la Serikali kupisha mijumuiko isiyo ya lazima, Eymael amekuwa akitoa program kupitia kwenye makundi yetu ya WhatsApp na wachezaji wanayafuata".

Kocha Eymael kwa sasa yupo nchini Ubelgiji, ambapo ameshindwa kurejea Tanzania kutokana na mipaka safari za ndege kuzuiwa Tanzania na mipaka kufungwa nchini Ubelgiji ili kujikinga na maambukizi zaidi ya virusi vya Corona.

Shirikisho la soka nchini TFF lilisimamisha shughuli zote za soka nchini Machi 17 baada ya Serikali kuzuia mikusanyiko ya watu kwa ajili ya kujikinga na virusi vya Corona, ambapo mpaka sasa haijulikani ni lini ligi zitarejea kufuatia Serikali kuongeza muda zaidi wa zuio.