Thursday , 12th Mar , 2020

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Gerson Msigwa, amesema familia ya Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa ilimuomba Rais Dkt John Pombe Magufuli, awasaidie kuchangia fedha kwa ajili ya kumlipia faini, ambapo amechangia Milioni 38, ikumbukwe kuwa mtoto wa Dada yake Msigwa amemuoa mtoto wa Rais.

Rais Dkt John Pombe Magufuli na Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa.

Akizungumza leo Machi 12, 2020, na EATV&EA Radio Digital,  Msigwa amesema kuwa wanafamilia wa Mbunge Msigwa walichangishana na kufikisha kiasi cha Shilingi Milioni Mbili na ndipo walipoamua kuomba Rais Magufuli aongeze nguvu.

"Mh Rais na Mchungaji Msigwa ni ndugu, hawa kina Msigwa wameoa nyumbani kwa Mh Rais, hao ndugu walichangishana hela jana wakaishia kupata Milioni 2, sasa ikabidi wamuombe Mh Rais awasaidie maana uwezo wa ndugu uliishia hapo na Mh Rais akachangia Milioni 38" amesema Msigwa.

Mbunge Mchungaji Peter Msigwa, alihukumiwa Machi 10, 2020, na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam, kulipa faini ya Shilingi Milioni 40 ama kifungo cha miezi mitano jela, katika kesi yake ya uchochezi iliyokuwa inamkabili pamoja na viongozi 7 wa CHADEMA.